JE NI SABABU ZIPI ZINAZOWEZA KUSABABISHA MAHAKAMA IKAMUONDOA MSIMAMIZI WA MIRATHI?
Mahakama inao uwezo wa kufuta haki ya usimamizi wa mirathi ikiwa kuna sababu za msingi za kufanya hivyo. Sheria imezitaja sababu hizo katika kifungu cha 49 kama ifuatavyo.
A] Kama mwenendo mzima wa kupata haki ya usimamizi wa mirathi ulikuwa na kasoro kubwa. Hivyo kuathiri kabisa usahihi wa kesi husika. Kwa mfano shauri hilo limefunguliwa kwenye mahakama ambayo haina mamlaka ya kusikiliza suala husika, kama muhusika amefariki mwanza halafu shauri likafunguliwa dare s salaam, au utolewaji wa mirathi ulifanywa bila kujumuisha watu ambao ilikuwa ni lazima wajumuishwe
B] kama mtu amepewa haki ya kusimamia mirathi kwa maoni yasiyo sahihi, kwa mfano pale ambapo wahusika wameghushi wosia au wametumia wosia ambao marehemu aliufuta wakati wa uhai wake
C] vile vile kama muhusika amepata usimamizi wa mirathi kwa kuelezea mambo yasiyo ya kweli, kwa mfano kusema uongo kuhusu mahali marehemu alikuwa akiishi au mahali mali zake zilipo, au pale ambapo mwanamke anasema yeye alikuwa ni mke wa marehemu wakati si kweli.
D]pale ambapo usimamizi wa mirathi umeonekana hauna maana tena au haufanyi kazi. Kwa mfano;
-pale ambapo mtu amepata usimamizi wa mirathi ikiaminika kwamba marehemu hakuacha wosia halafu wosia halisi umepatikana au
-pale mtu aliyepewa usimamizi wa mirathi amekuwa hana akili timamu,
-au pale ambapo usimamizi wa mirathi umekamilika huwezi tena kufuta usimamizi hata kama wosia utapatikana.
E] Pale ambapo msimamizi wa mirathi kwa makusudi ameshindwa kuleta orodha ya mali za marehemu na jinsi alivyozishughulikia.
Sababu ambazo haziwezi kufanya usimamizi wa mirathi ufutwe ni pamoja na
I] kutoelewana kwa kawaida kati ya wasimamizi wa mirathi.
Ii] Kuacha kuleta orodha ya mali za marehemu bila kukusudia.
Jungu Attorneys at Jungu La Sheria Tanzania.

0 Maoni
WEKA MAONI YAKO HAPA.
TAFADHALI USITUMIE LUGHA YA MATUSI AU KUUDHI KWANI NI KOSA KISHERIA.
KARIBU SANA NA ASANTEE.. 🇹🇿