Ticker

6/recent/ticker-posts

Haki za kisheria za wanufaika watarajiwa wa mirathi, na Johnson Yesaya


 

JE WATU WANAOTARAJIA KUFAIDIKA NA MIRATHI WANA HAKI ZIPI ZA KISHERIA KUFUATILIA USIMAMIZI WA MIRATHI?


I] HAKI YA KUMTAKA MSIMAMIZI ASIMAMIE MIRATHI AU AJIONDOE

Haki hii anayo mtu yeyote mwenye maslahi na mirathi ya marehemu, ambapo anaweza kumtaka aje mahakamani na kufanya zoezi la usimamizi wa mirathi au ajiondoe katika usimamizi kama aliteuliwa kwa wosia au na ukoo. Hii mara nyingi hutokea pale ambapo msimamizi wa mirathi bila sababu za msingi anachelewesha kufungua mirathi na mali za marehemu zinaendelea kupotea bure. Muhusika asipotokea mahakamani itachukuliwa kwamba amekataa uteuzi uliofanywa katika wosia wa usimamizi wa mirathi. Ni vizuri kuchukua hatua hii mapema lakini kwa umakini kwa kuwa katika kipindi hiki inaweza kutokea msimamizi huyu akaenda mahakamani kimya kimya akapata uthibitisho wa mahakama na akachezea mali za marehemu na warithi wakabaki wanateseka.


ii] HAKI YA KUWEKA PINGAMIZI

Mtu yeyote ambaye anaona ana haki au ana maslahi na mirathi ya marehemu anaweza kuweka pingamizi mahakamani dhidi ya mtu ambaye anaomba kupewa usimamizi wa mirathi. Lengo la kuweka pingamizi ni kuiambia mahakama kwamba mtu aliyeomba kupewa usimamizi wa mirathi asipewe haki hiyo mpaka mtu aliyetoa pingamizi apewe taarifa.

Pingamizi hili linaweza kuwa na sababu mbalimbali ikiwamo kuangalia kama wosia unauhalali, uaminifu wa muhusika na tabia yake kwa ujumla. Haitarajiwi familia ikubali mtu mwenye historia ya jinai apewe usimamizi. Pingamizi hili litakuwa na nguvu ya kisheria kwa muda wa miezi minne na baada ya hapo lazima liwekwe pingamizi jingine ili kulipa uhai lile la kwanza. Baada ya hapo mahakama husikiliza pingamizi hilo.


iii]HAKI YA KUKAGUA MAENDELEO YA KAZI YA USIMAMIZI WA MIRATHI

Mtu yeyote anayetarajia kufaidika na mali za marehemu kutokana na wosia au hata kama hakuna wosia au mtu yeyote anayemdai marehemu ana haki ya kukagua listi ya mali iliyopelekwa mahakamani na msimamizi wa mirathi. Hii husaidia kuepusha udanganyifu unaofanywa na wasimamizi wengi wa mirathi kwa kuficha baadhi ya mali za marehemu.


iv] MGAO WAKE HALALI

Warithi wana haki ya kupata mgao wao halali wa mali kama ilivyoonyeshwa na wosia wa marehemu au kutokana na taratibu za kimila au kidini zinazokubalika kisheria.

Jungu Attorneys at Jungu La Sheria Tanzania.

Chapisha Maoni

0 Maoni