SHERIA IMEWAPA WAJIBU UPI WASIMAMIZI WA MIRATHI?
Kazi ya usimamizi wa mirathi ni kazi ambayo inahitaji uaminifu wa hali ya juu, tuangalie mamlaka ya msimamizi wa mirathi.
1.Huyu atakuwa ndio muwakilishi halali wa kisheria wa mambo yote ya marehemu na mali zote za marehemu kisheria zitakuwa chini yake kama msimamizi na sio kwamba ni mali yake, katika kesi ya-MOHAMED HASSAN Vs MAYASA MZEE na MWANAHAWA MZEE [1994] T.LR 225 mahakama ya rufaa iliamua kwamba kisheria msimamizi wa mirathi halazimiki kupata ruhusa ya warithi kabla ya kuuza mali yoyote ya marehemu.
-Katika kesi ya AZIZ DAUDI AZIZ Vs AMIN AHMED ALLY & ANOTHER CIV. App No 30 of 1990 [unreported] mahakama ya rufaa iliamua kwamba pale tu msimamizi wa mirathi anapoteuliwa, mali zote zinakuwa chini ya mamlaka yake kama msimamizi na anachukua majukumu ambayo alikuwnayo marehemu kwenye mali yake wakati yu hai. Msimamizi huyu huachiwa kuamua jinsi ya kushughulikia mirathi hiyo kadri atakavyoona inafaa.
2. Atakuwa na mamlaka ya kufungua mashitaka mahakamani kwa niaba ya marehemu au kushitakiwa kwa niaba ya marehemu na atawajibika kulipa madeni ya marehemu kutoka katika mali alizoacha marehemu.
3.Msimamizi wa mirathi vile vile atakuwa na uwezo wa kuhamisha umiliki wa mali za marehemu kama atakavyoona inafaa kwa kuziweka rehani, kuziuza au kuzikodisha, kwa kuzingatia maslahi ya warithi na watu wanaomdai marehemu. Hivyo msimamizi wa mirathi hawezi tu kuamka na kutangaza kuuza mali za marehemu bila sababu za msingi.
4. Atawajibika kutumia kiasi Fulani cha pesa za marehemu kwaajili ya kutunza mali za marehemu ziwe katika hali nzuri na zisiharibike.
5. Msimamizi wa mirathi anatakiwa ndani ya miezi sita tangu apewe usimamizi au ndani ya muda mahakama ambao itaona unafaa, anatakiwa apelike mahakamani na kuonyesha mali zote za marehemu na thamani yake halisi, madeni yake anayodaiwa au anayodai marehemu na ndani ya mwaka mmoja msimamizi wa mirathi atatakiwa tena kama mahakama itakavoona inafaa, aonyeshe mali za marehemu zilizo mikononi mwake na jinsi alivyozifanya au kuzishughulikia.
Mahakama ina uwezo wa kuendelea kumuongezea muda muhusika kadri itakavyoona inafaa. Lakini kama msimamizi wa mirathi atatakiwa na mahakama kuonyesha mali za marehemu na akashindwa kufanya hivyo ndani ya muda aliopewa, atakuwa ametenda kosa la jinai na akipatikana na hatia atatakiwa alipe faini ya shilling elfu mbili au apewe kifungo cha miezi sita.
Na kama ataonyesha mali hizo kwa nia ya kudanganya au kuficha atakuwa ametenda kosa la jinai ambalo kifungo chake ni miaka saba. Mtu yeyote mwenye maslahi na mirathi anaouwezo wa kufanya ukaguzi ili kujiridhisha na usimamizi wa mirathi ya marehemu
6. Msimamizi wa mirathi vile vile anatakiwa akusanye mali za marehemu na madeni aliyokuwa akidai na kulipa madeni aliyokuwa akidaiwa, Katika madeni aliyokuwa anadai marehemu ni vizuri msimamizi wa mirathi akayadai mapema ili yasije yakapitwa na wakati kisheria
Msimamizi wa mirathi hatakiwi kujipatia faida kutokana na usimamizi wa mirathi hiyo, na kama msimamizi wa mirathi yeye mwenyewe au kwa kupitia kwa mtu mwingine atanunua mali ya marehemu, uuzaji huo unaweza kukataliwa kisheria na mtu yeyote mwenye maslahi na mirathi hiyo . Moja ya sababu ya kufanya hivyo ni kwamba kuna uwezekano mkubwa akajiuzia mali hizo kwa bei ya chini kuliko thamani halisi ya mali husika.
7. Vile vile ni jukumu la msimamizi wa mirathi kutoa fedha kwaajili ya shughuli za mazishi ya marehemu, ila gharama hizo ziangalie hali halisi ya maisha ya marehemu na kama ameacha kiasi cha mali cha kutosha kwaajili ya shughuli hiyo. Kama msimamizi wa mirathi alitoa fedha yake kwaajili hiyo ana hakiya kwanza ya kulipwa fedha zake kabla ya madeni mengine ya marehemu.
Jungu Attorneys at Jungu La Sheria Tanzania.

0 Maoni
WEKA MAONI YAKO HAPA.
TAFADHALI USITUMIE LUGHA YA MATUSI AU KUUDHI KWANI NI KOSA KISHERIA.
KARIBU SANA NA ASANTEE.. 🇹🇿