JINAI
Kwa hakika wengi wetu tumewahi kusikia neno Jinai hasa katika masuala mbalimbali ya kisheria, kwa hapa Tanzania, Jinai ni aina ya kosa au makosa ya kisheria ambayo husimamiwa na Jamhuri au serikali na yanapotendeka mlalamikaji mahakamani huwa ni Jamhuri dhidi ya mtenda kosa. Kesi za Jinai hupelekwa na kufunguliwa mahakamani na Jamhuri ambayo ni serikali kumshtaki mtu ambaye amefanya kosa hilo, mfano wa makosa ya Jinai ni kama wizi, ubakaji, ulawiti, ujambazi, rushwa, mauaji, makosa ya mtandao na mengine mengi.
Sheria zenye makosa ya Jinai ni nyingi mfano Kanuni ya adhabu sura 16, sheria ya rushwa, sheria ya makosa ya mtandao na sheria zinginezo, katika kusimamia na kushughulikia makosa ya Jinai kuna sheria inayoitwa sheria ya mwenendo wa makosa ya Jinai, sheria hii inatoa mwongozo wa namna ya kukamata watuhumiwa wa makosa ya Jinai, namna ya kuandaa nyaraka mbalimbali za kisheria kama fomu za mashtaka na zinginezo nyingi na taratibu zote zinazotakiwa kufanywa na polisi wakati wa kuendesha mashtaka mahakamani.
Jinai hupelekwa mahakamani na polisi ambao wao hukusanya ushahidi ambao watautumia mahakamani kuthibitisha madai yao mbele ya mahakama dhidi ya mtuhumiwa, polisi huwa mashahidi, lakini watu wengine wanaweza kuwa mashahidi endapo watakuwa na uhusika wa namna fulani na tukio lililotokea, yawezekana walishuhudia uhalifu huo au ni watu wenye taaluma fulani ambao wanaweza kueleza mazingira ya tukio kuhusianisha na tukio lenyewe.
ADHABU ZA JINAI
Kanuni ya adhabu sura ya 16 kifungu cha 25, kinatoa orodha ya adhabu zinazoweza kutolewa kwa mtu ambaye amekutwa na hatia mahakamani, miongoni mwa adhabu hizo ni adhabu ya kifo, kifungo cha maisha, kutozwa faini, adhabu ya viboko, adhabu ya kutunza amani, na adhabu zinginezo nyingi. Hizi ndizo adhabu kuu ambazo mara nyingi hutolewa na mahakama endapo mtuhumiwa atakutwa na hatia ya kosa au makosa ya jinai. Adhabu za makosa ya Jinai zinaweza kutolewa kwa mtu mmoja au kwa kundi la watu wengi endapo watuhumiwa walifanya kosa moja wakiwa wengi.
Mfano kosa la kubaka au kuua linaweza kufanywa na mtu mmoja au kundi, endapo kosa la Jinai litafanywa na watu wengi, kesi huwa ni moja na watuhumiwa zaidi ya mmoja wanaweza kuhukumiwa kwenda jela kwa kosa moja na adhabu ya kufanana kutokana na mazingira ya uhalifu wenyewe. Lakini pia watuhumiwa wengi wanaweza kutuhumiwa kwa kufanya kosa moja lakini kila mtuhumiwa anaweza kupewa adhabu tofauti kutokana na namna ya ushiriki wao katika uhalifu wenyewe.
kama kuna kitu kuhusu jinai ulitaka kukifahamu na hakijaongelewa hapa unaweza kuwasiliana nasi kwa kutumia mawasiliano yetu.
Jungu Attorneys at Jungu La Sheria Tanzania.

0 Maoni
WEKA MAONI YAKO HAPA.
TAFADHALI USITUMIE LUGHA YA MATUSI AU KUUDHI KWANI NI KOSA KISHERIA.
KARIBU SANA NA ASANTEE.. 🇹🇿