Ticker

6/recent/ticker-posts

MADAI

MADAI

Umewahi kusikia madai au kesi ya madai? Katika aina za kesi kuna kesi za jinai na madai, kesi za madai ni zile ambazo zinakuwa hazihusishi ujinai ndani yake ila hutokana na migogoro au hasara za kibiashara pamoja na kudai fidia kutokana na kusababishiwa madhara Fulani na mtu mwingine. Mara nyingi kesi hizi huhusisha watu binafsi, taasisi au serikali dhidi ya taasisi na kinyume chake.

Kesi hizi za madai mara nyingi huhusiana na mambo ya MIKATABA, NDOA, KAZI, BIASHARA, ARDHI, MIRATHI, MADHARA, na mengineyo mengi. Kesi hizi hufunguliwa na mtu/watu binafsi dhidi ya mtu/watu binafsi, taasisi, shirika au serikali na kinyume chake. Katika kesi hizi mara nyingi lengo huwa ni FIDIA kutokana na madhara au hasara aliyoipata mwathirika.

MFANO

Kampuni A imeingia katika mkataba na kampuni B, mkataba huu ni wa ujenzi wa jengo la kampuni B, kampuni B inalipa fedha nusu za ujenzi wa jengo kwa kampuni A, makubaliano ni kuwa jengo likamilike kwa mwaka mmoja ndipo zilipwe fedha zilizosalia, baada ya mwaka mmoja jengo linakamilika lakini kampuni B inashindwa kumalizia kiasi cha fedha zilizosalia kama deni, KAMPUNI A INAFUNGUA KESI YA MADAI KUDAI DENI LILILOSALIA.

Katika kesi za madai, mtu binafsi anaweza kuishtaki SERIKALI endapo kuna vitendo visivyo vya halali vimefanywa na serikali dhidi ya mtu huyo na kumsababishia HASARA, ni jambo la kawaida sana kuishtaki serikali inapofanya mambo yanayotia hasara kwa waathirika. KUISHTAKI SERIKALI SI KUSHINDANA NA SERIKALI, NI HAKI.

ADHABU KATIKA KESI ZA MADAI

Mara nyingi adhabu za kesi za madai ni FIDIA, kesi zinazohusu NDOA NA MIRATHI mara nyingi huhitaji mgawanyo sahihi wa mali. Katika kesi ya madai ni nadra sana kukutana na hukumu ya kifungo jela japokuwa inawezekana endapo utapewa adhabu ya kulipa fidia na ukashindwa, adhabu hiyo huhama na kuwa ya kifungo (kwa mtu binafsi) endapo ni taasisi imeshindwa kulipa fidia, mali zake zinaweza kushikiliwa na baadae kutaifishwa au kuuzwa kwa lengo la kupata fedha za kumlipa mwathirika

Jungu Attorneys at Jungu La Sheria Tanzania.

Chapisha Maoni

0 Maoni