NAMNA ZA UTOAJI WA MAMLAKA YA USIMAMIZI WA MIRATHI TANZANIA.
Namna ya kutoa usimamizi wa mirathi hutegemea jinsi marehemu alivyojiandaa kukutana na kifo chake, kuna wengine huacha wosia na wengine huwa hawaachi wosia.
A] KAMA KUNA WOSIA
Kama kuna wosia, usimamizi wa mirathi hupewa mtu yule tu aliyetajwa kwenye wosia, mtu huyo anaweza kuwa ametajwa moja kwa moja au kwa hali halisi ilivyojionyesha kwenye wosia kwamba lazima atakuwa ni yeye. Hivyo kuandika wosia ni nafasi pekee ya kuchagua msimamizi wa mirathi.
Vile vile mtoa wosia anaweza kuchagua mtu zaidi ya mmoja kusimamia mirathi yake. Ikumbukwe kuwa kuna wosia za aina mbili. Ya kwanza ni wosia wamaandishi na wa pili ni ule wa maneno. Wosia wa maneno ni lazima uthibitishwe kwa ushahidi wa wahusika ambao ulitolewa mbele yao. Pale ambapo mahakama itajiridhisha na uwepo wa wosia na ikatoa amri ya usimamizi Itakuwa imethibitisha usahihi wa wosia husika. Wosia wamaandishi nao lazima uthibitishwe angalau kwa kuleta mtu aliyeshuhudia ukiandikwa ili athibitishe kwamba marehemu alikuwa na akili timamu wakati akiandika wosia huo na hakulazimishwa na mtu yeyote.
B] WOSIA ULIOMBATANISHWA NA BARUA YA USIMAMIZI WA MIRATHI
Hii hutokea katika mazingira yafuatayo
i] Pale ambapo marehemu ameacha wosia lakini wosia huo hauja mtaja mtu ambaye marehemu alitaka awe msimamizi wa mirathi yake
ii] Pale ambapo watu wote waliotajwa na marehemu katika wosia kwamba wasimamie mirathi yake wamekataa hoja hiyo au ni watu ambao kisheria hawana uwezo wa kusimamia mirathi, kwa mfano mtoto, mtu asiye na akili timamu n.k
iii] Pale ambapo wasimamizi wote wa mirathi walitajwa katika wosia wamefariki kabla mwandika wosia hajafariki au amefariki kabla ya kumaliza kazi yake ya usimamizi wa mirathi. Katika hali kama hii, lazima ndugu wakae wachague mtu ambaye wamempendekeza kuwa msimamizi wa mirathi na watatakiwa waende mahakamani na wosia huo ili wakaombe mahakama imthibitishe rasmi. Hapa ndipo amri ya usimamizi wa mirathi ukiwa na wosia ulioambatanishwa na barua ya usimamizi wa mirathi hutolewa.
C] KAMA HAKUNA WOSIA
Kama marehemu hakuacha wosia wowote, barua za usimamizi wa mirathi zinaweza kutolewa kwa mtu yoyote ambaye kwa mujibu wa taratibu za usimamizi wa mirathi zinazohusika katika mirathi hiyo [za kimila au zakiserikali au zakiislamu] atakuwa ana haki ya kupata mali zote za marehemu au sehemu ya mali hizo.
Pale inapotokea mtu zaidi ya mmoja ameomba usimamizi wa mirathi ya marehemu, mahakama itakuwa na utashi wa kuchagua mmoja au mtu zaidi ya mmoja kusimamia mali za marehemu, na katika kufanya hivyo mahakama inatakiwa kisheria iangalie mtu mwenye maslahi makubwa zaidi na ya karibu na mirathi hiyo kuliko yule mwenye maslahi madogo.
Vile vile kama itatokea kwamba marehemu alikuwa anadaiwa, na hakuna ndugu aliyefungua mirathi ya marehemu mahakamani, basi mdai ana uwezo wa kuomba kufungua mirathi husika, Mahakama inapoona kwamba ni muhimu au ni busara kumchagua mtu ambaye katika hali ya kawaida asingechaguliwa kusimamia mirathi, mahakama, kwa kuangalia ukaribu wa kiundugu, maslahi aliyonayo muhusika katika mirathi, usalama wa mirathi husika na uwezekano wa mirathi hiyo kusimamiwa vyema, itamchagua mtu huyo.
Jungu Attorneys at Jungu La Sheria Tanzania.

0 Maoni
WEKA MAONI YAKO HAPA.
TAFADHALI USITUMIE LUGHA YA MATUSI AU KUUDHI KWANI NI KOSA KISHERIA.
KARIBU SANA NA ASANTEE.. 🇹🇿