TALAKA (DIVORCE)
Leo tujifunze juu ya talaka, maana ya taraka na chombo chenye mamlaka kisheria kutoa talaka. Pia tutajifunza sababu na mambo yanayokubaliwa kisheria ili talaka iweze kutolewa. Wakati mwingine sababu hizo huwepo lakini wana ndoa huamua kutengana; hivyo basi tutajifunza juu ya kutengana. Pamoja na hayo yote tutajifunza taratibu za kufuata kabla ya talaka kutolewa.
MAANA YA TALAKA
Sheria inayosimamia masuala ya talaka ni sheria ya Ndoa ya mwaka 1971. Na kwa mujibu wa sharia hiyo, “Talaka ni ruhusa ya kisheria ambayo mume au mke hupewa wakati anapomwacha mwenzie
CHOMBO CHENYE MAMLAKA YA KUTOA TALAKA
Chombo pekee chenye uwezo wa kuvunja ndoa ni mahakama. Kwa kawaida mahakama hutoa talaka kwa ndoa ambayo imedumu kwa kipindi cha miaka miwili au zaidi. Lakini mahakama inaweza kutoa talaka hata kama ndoa haijadumu kwa kipindi hicho cha miaka miwili iwapo mlalamikaji atatoa sababu nzito sana.
Kutengana
Kutengana si talaka. Kutengana maana yake ni mume na mke kuishi mbalimbali. Kutengana kunaweza kuwa kwa mapatano kati
ya mume na mke bila ya kufika mahakamani.
Aidha kutengana
kunaweza kutokana na amri ya mahakama kuwatenganisha
wanandoa ikiwa mmoja wao atakuwa amepeleka ombi hili mahakamani. Faida ya kutengana ni kuwa mume, mke au wote wawili baada ya muda, huweza kutambua makosa yao na hatimaye kurudiana na kuendelea kuishi pamoja.
KUTENGANA KWA MAPATANO
Mume na mke kwa hiari yao wanaweza kukubaliana watengane ikiwa wameona hawaelewani katika maisha yao. Mapatano yanaweza kuwa ya mdomo au ya maandishi. Mambo ya kuzingatia kwenye mapatano ni:-
a) Mume na mke wote wameridhia kuisha mbalimbali
b) Kutokuudhiana, yaani hakuna ambaye atakwenda kumghasi mwenziwe au kutaka kujamii ana naye.
c) Mapatano ya matumizi kwa mke na watoto wa ndoa kama wapo
d) Mke kuishi maisha ya heshima; (mume je?)
e) Kama kuna watoto, mapatano yaeleze ni nani atakaa na watoto
f) Kama kuna mali ya pamoja, lazima kuwe na mapatano kuhusu mali hiyo
KUTENGANA KWA AMRI YA MAHAKAMA
Sababu ambayo inaweza kuifanya Mahakama kutoa amri ya kutengana ni ile ile ya kuwa ndoa imevunjika. Ushahidi wa kuonyesha kuvunjika kwa ndoa ni ule ushahidi unaotakiwa katika talaka. Lakini mahakama inapotoa amri ya kutengana si lazima iamini kuwa ndoa imevunjika kiasi ambacho haiwezi kurekebishwa. Mahakama ikishatoa amri ya kutengana inaweza pia kutoa amri mume ampe mke na watoto kama wapo kiasi fulani cha matumizi.
SABABU YA KUTOA TALAKA NI ZIPI?
Mahakama hufikia uamuzi wa kutoa talaka baada ya kuridhika kuwa ndoa imevunjika kiasi ambacho haiwezi kurekebishika tena.
Mambo yanayofanya ndoa ionekane kuwa imevunjika kiasi ambacho haiwezi kurekebishika tena ni:-
a) Ugoni
Ugoni ni zinaa kati ya mwanamume na mwanamke ambao hawajaoana, aidha mwanamume akiwa na mke wake au mwanamke akiwa ni mke wa mtu. Ili ugoni uwepo ni lazima
kitendo cha zinaa kiwe cha hiari
b) Ukatili
Ukatili unakuwepo pale ambapo mlalamikaji ameumizwa mwili au kuharibiwa afya yake, au kuwa na hofu ya kuamini kwamba hapo baadaye ataumizwa mwili au afya yake.
c) Kulawiti
Kulawiti maana yake ni kumwingilia mtu kinyume na maumbile.
d) Kichaa
Ili talaka iweze kutolewa ni lazima madaktari wawili bingwa wa magonjwa ya akili wathibitishe kuwa ugonjwa huo hautapona
e) Kifungo
Ikiwa mume au mke ametenda kosa la jinai na ameonekana ana hatia ya kosa hilo, iwapo atafungwa kifungo cha maisha au kwa muda usiopungua miaka 5 talaka inaweza kutolewa kwa sababu hiyo.
f) Uasi (Utoro)
Kuasi katika lugha ya sheria ya talaka ni mume au mke kuhama kutoka nyumba ya ndoa na kwenda kuishi mahali pengine bila sababu yoyote. Wakati mwingine mke huondoka kutokana na vitendo vya ukatili anavyofanyiwa na mume wake. Kisheria hapa mume ndiye aliyemwasi mke. Huu ndio unaoitwa “uasi wa hila”. Kitendo cha uasi kikithibitika ni ushahidi wa kuonyesha kuwa ndoa imevunjika.
g) Kutengana
Ikiwa mume na mke wametengana kwa muda usiopungua miaka 3, (au zaidi) kutengana kwao kutakuwa ni ushahidi kuonyesha kwamba ndoa imevunjika.
TARATIBU ZA KUFUATA WAKATI WA KUVUNJA NDOA
1. Nenda Baraza la Usuluhishi la ndoa linalotambuliwa kisheria kwa mfano, BAKWATA, Kanisani au Baraza la sharia la Kata.
2. Baraza la Usuluhishi likishindwa kusuluhisha, litatoa hati kuelezea maoni yake na kuelekeza shauri likatatuliwe Mahakamani.
3. Andika madai yakuvunja ndoa na uyawasilishe Mahakani ukiambatanisha cheti cha ndoa kama kipo, hati ya Baraza la Usuluhishi na hati yoyote ile ambayo ungependa Mahakama iione.
Jungu Attorneys at Jungu la sheria Tanzania.

0 Maoni
WEKA MAONI YAKO HAPA.
TAFADHALI USITUMIE LUGHA YA MATUSI AU KUUDHI KWANI NI KOSA KISHERIA.
KARIBU SANA NA ASANTEE.. 🇹🇿