Kifungu hicho kinaanzisha mahakama inayojulikana kama Mahakama ya Watoto, kwa madhumuni ya kusikiliza na kuamua masuala yanayohusiana na watoto.
Jaji Mkuu anaweza, kwa notisi itakayochapishwa kwenye Gazeti la Serikali, kuteua jengo lolote linalotumiwa kama mahakama ya mwanzo kuwa Mahakama ya Watoto. Hakimu Mkazi atapewa jukumu la kusikiliza mashauri katika Mahakama ya Watoto.
Mahakama ya Watoto itakuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuamua-
(a) mashtaka ya jinai dhidi ya mtoto; na
(b) maombi yanayohusiana na malezi, matunzo na ulinzi wa mtoto.
Mahakama ya Watoto itakuwa pia na mamlaka na uwezo utakaotolewa kwake na sheria nyingine yoyote.
Mahakama ya Watoto, pale itakapowezekana, itakaa katika jengo tofauti na jengo ambalo kwa kawaida hutumika kusikiliza kesi za watu wazima.
Utaratibu wa kuendesha mashauri katika Mahakama ya Watoto katika masuala yote utakuwa ni kulingana na kanuni zitakazotungwa na Jaji Mkuu kwa madhumuni hayo, lakini kwa namna yoyote zitakuwa ni kulingana na masharti yafuatayo-
(a) Mahakama ya Watoto itakaa mara nyingi kama itakavyo lazimu;
(b) mashauri yataendeshwa kwa faragha;
(c) kwa kadri itakavyowezekana mashauri yataendeshwa kwa njia isiyo rasmi, na yataendeshwa kwa kuuliza maswali bila kumweka mtoto katika taratibu ngumu za kisheria.
(d) Afisa Ustawi wa Jamii atahudhuria;
(e) mzazi, mlezi au mtu anayemwakilisha mtoto watakuwa na haki ya kuhudhuria;
(f) mtoto atakuwa na haki ya kuwa na ndugu wa karibu na kuwakilishwa na wakili;
(g) haki ya kukata rufaa itawekwa bayana kwa mtoto; na
(h) mtoto atakuwa na haki ya kujieleza na kutoa maoni.
Mbali ya wajumbe na maafisa wa Mahakama ya Watoto, watu wafuatao tu, kwa ridhaa ya mahakama, wanaweza kuhudhuria kikao chochote cha Mahakama ya Watoto-
(a) wahusika wa kesi iliyoko mbele ya mahakama, mawakili wao, mashahidi na watu wengine ambao wamehusika moja kwa moja au wameshiriki katika kesi; na
(b)mtu mwingine yeyote ambaye mahakama itamruhusu kuwepo.

0 Maoni
WEKA MAONI YAKO HAPA.
TAFADHALI USITUMIE LUGHA YA MATUSI AU KUUDHI KWANI NI KOSA KISHERIA.
KARIBU SANA NA ASANTEE.. 🇹🇿