Ticker

6/recent/ticker-posts

MAELEZO YA ONYO (MAELEZO YA MTUHUMIWA). Na JOHNSON YESAYA. LL.B.



Maelezo ya onyo, "cautioned statement" ni maelezo ambayo hutolewa kituo cha polisi na mtuhumiwa wa kosa la jinai baada ya kuwa amefahamishwa na afisa wa polisi anayemhoji kwamba, "halazimiki  kujibu  swali  lolote  atakaloulizwa na  afisa  polisi,  tofauti  na  swali linalotafuta  habari  kuhusiana  na  jina  na anuani  yake", na "anaweza  kukataa kujibu swali  lolote  atakaloulizwa  na afisa polisi". Na kwamba maelezo yake yanaweza kutumiwa kama sehemu ya ushahidi mahakamani.


Baada ya hatua hiyo, mtuhumiwa anaweza kutoa maelezo yake kwa njia ya mdomo kisha kuandikwa na afisa wa polisi, au anaweza kuandika maelezo hayo kwa mkono wake na kukabidhi kwa afisa wa polisi.


Baada ya maelezo kuchukuliwa kwa maandishi, afisa wa polisi atalazimika kuyasoma maelezo hayo kwa mtuhumiwa au kufanya maelezo hayo yasomwe kwa mtuhumiwa, au kumpa mtuhumiwa asome maelezo aliyoyatoa, Kisha mtuhumiwa anaweza kurekebisha makosa katika maelezo yake.


Mtuhumiwa atasaini maelezo yake kuthibitisha kuwa ameyasoma maelezo hayo, mtuhumiwa hatakiwi kutoa maelezo kwa kulazimishwa kwa kupigwa au njia yoyote nyingine tofauti na njia za kisheria.


Pale  mtu  anapokuwa  kizuizini, afisa  polisi  hatamuuliza maswali  yoyote,  au  kumtaka  kufanya  chochote,  kwa  madhumuni yanayohusiana  na  upelelezi  wa  kosa, isipokuwa  kama:– 


(a) afisa  polisi  amemwambia  jina  na  cheo  chake;


(b) mtu  huyo  amejulishwa  na afisa  polisi,  katika  lugha ambayo  anaielewa,  kwa maandishi  na,  kama inawezekana,  kwa  mdomo,  kwamba  yuko  kizuizini  na kosa  ambalo kwalo  yupo  kizuizini;  na  mtu  huyo  ameonywa  na  afisa  polisi  katika  hali  ifuatayo, yaani,  kwa  kumjulisha  au  kusababisha  kujulishwa, katika  lugha  anayoielewa,  kwa  maandishi  kwa  kufuata fomu  iliyowekwa  na,  iwapo  inawezekana,  kwa  mdomo kwamba;


(i)  halazimiki  kujibu  swali  lolote  atakaloulizwa na  afisa  polisi,  tofauti  na  swali linalotafuta  habari  kuhusiana  na  jina  na anuani  yake;  na


(ii) kwa  kuzingatia  Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, anaweza kuwasiliana  na  mwanasheria,  ndugu  au rafiki.

Chapisha Maoni

0 Maoni