Ticker

6/recent/ticker-posts

JAJI KIONGOZI NI NANI?



KATIBA YA TANZANIA

IBARA YA 109.-(1) inasema,  Kutakuwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu (ambaye katika ibara zifuatazo kwenye Katiba atatajwa tu kwa kifupi kama "Jaji Kiongozi") na Majaji wengine wa Mahakama Kuu wasiopungua kumi na watano.

(2) Jaji Kiongozi na Majaji wengineo wa Mahakama Kuu watateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Tume ya Kuajiri ya Mahakama.

(3) Bila ya kuathiri masharti ya Katiba hii au sheria nyingine yoyote kuhusu madaraka ya Jaji Mkuu aliyetajwa katika ibara ya 118, Jaji Kiongozi atakuwa ndiye msaidizi maalum wa Jaji Mkuu katika utendaji wa kazi katika Mahakama Kuu na Mahakama nyinginezo zote za ngazi ya chini yake, na katika madaraka hayo Jaji Kiongozi atatekeleza kazi na shughuli atakazoagizwa au kuelekezwa mara kwa mara na Jaji Mkuu, na kwamadhumuni ya ibara hii, Jaji Kiongozi atajulikana pia kama Mkuu wa Mahakama Kuu.

(4) Mbali ya madaraka yake ya kawaida ya Jaji wa Mahakama Kuu kama Majaji wengine wote wa Mahakama Kuu, Jaji Kiongozi atakuwa pia na mamlaka ya kutekeleza kazi na shughuli zote zinazoambatana na mamlaka ya Mahakama Kuu ambazo kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au ya sheria nyingine yoyote au kufuatana na mila za kisheria zinazotumika hutakiwa zitekelezwe na Mkuu wa Mahakama Kuu: Isipokuwa kwamba masharti ya ibara hii ndogo hayatatumika kwa ajili ya utekelezaji wa kazi au shughuli ambazo kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au ya Sheria nyingine yoyote au kufuatana na mila za kisheria zinazotumika Tanzania zimetajwa mahususi au zinafahamika kuwa ni kazi au shughuli zinazotakiwa kutekelezwa tu na Jaji Mkuu.

(5) Kwa madhumuni ya kuondoa mashaka juu ya ufafanuzi au utekelezaji wa masharti ya ibara ndogo ya (3) na ya (4) ya ibara hii, inatamkwa rasmi hapa kwamba isipokuwa kama masharti ya Katiba hii au ya sheria nyingine yoyote yameagiza vingine, Jaji Mkuu atakuwa na uwezo wa kutoa kwa Jaji Kiongozi mara kwa mara maagizo au maelekezo kuhusu utendaji wa kazi na shughuli zake kama Mkuu wa Mahakama Kuu: vile vile, Jaji Mkuu atakuwa na uwezo wa kuwakilisha kwa Jaji Kiongozi baadhi ya madaraka yake ya uongozi na usimamizi juu ya utekelezaji wa kazi katika 

Mahakama Kuu na Mahakama nyinginezo zote za ngazi ya chini yake, na kila inapohitajika, Jaji Mkuu anaweza kutekeleza yeye mwenyewe moja kwa moja madaraka yake yoyote aliyowakilisha kwa Jaji Kiongozi.

Chapisha Maoni

0 Maoni